@DennisShonko LALA PEMA PROF. KEN WALIBORA: INGAWA UMEONDOKA, HUTAFUTIKA MOYONI MWANGU.

Ulikuwa uvumi tu! Ufifi!

IMG_20200415_141522

Jumanne usiku, kila nilipopenyepenya kwenye mitandao ya kijamii niliwaona wengi wakikutajataja. Walikutajataja kwa kile ambacho nilikataa kabisa kuamini. Wengi hatukuamini na hivyo kutugeuza wakosoaji. Tuliwaonya ‘kasuku’ dhidi ya uvumi kuwa ulikuwa umetangulia mbele ya haki. Ili nisiutese moyo wangu nilizima data hadi keshoye Jumatano, 15/4/2020. Nikawa ninachakura kwenye Twitter, Whatsapp na Facebook. ‘Uvumi’ ulikuwa umetamba kote. Sikutaka ya kukisiwa tena! Nilipoiwasha televisheni, duh! Stesheni ya NTV ilikuwa na maandishi haya kwenye kiwambo: 

“BREAKING NEWS: PROF. KEN WALIBORA IS DEAD. RENOWNED AUTHOR AND JOURNALIST WAS HIT BY A MATATU ALONG LANDHIES ROAD ON FRIDAY.”

Skrubu zangu za miguu zilifunguka. Mtima ulidunda mara elfu sijui kama ngoma za wapi! Sijui ni kwa nini kilipita kitambo kabla ya habari hizo kuniingia na kunikaa akilini licha ya kuwa na ushahidi (wengi walikuwa washaanza kutoa na kutuma rambirambi zao). Siku tano! Siku tano zilikuwa zimepita tangu utupe mkono. Iweje?

Hayo kando!

sew

Prof. Nakumbuka vizuri sana tulianza kuwasiliana kwenye Facebook. Binafsi nilikuwa nimekusoma tangu kitambo, hapa nikikumbuka riwaya yako ya Siku Njema. Mengi yaliandikwa kukuhusu kwenye mitandao. Nilikutazama kwenye runinga na kukusikiliza kwenye redio, hivyo, sikuhitaji kukuuliza ‘Prof. Ken Walibora ni nani?’

“Mimi ni Dennis Sh…” nilijaribu kujitambulisha kwako.
“Shonko, nakujua sana,” ulinikata kalima. Nilibaki mdomo wazi kama kasiba. Nilishangaa ulijuaje niliipenda lugha ya Kiswahili. Kumbe ulikuwa ulikuwa unazisoma posti zangu kwenye Facebook!

Urafiki ukapata mizizi.

Baadaye ulinipa namba zako ili kurahisisha mawasiliano yetu. Nilipokuomba unishike mkono katika uandishi hukusita kukubali. Nilishukuru. Ulinishauri kila nilipokukimbilia. Nilipoona kuwa nilikuwa nimejaribu kukupigia simu, ulinipigia. Hukuzipuuza jumbe zangu. Huo ndio utu, si kutu! Msomaji, hebu nikuulize, wangapi wenye vyeo na hali hufanya hivyo?

Ilipita miaka ayami ya kutamani tuonane ana kwa ana ikiwa si kupokezana mikono. Siku ya Mungu ilifika. Ulinitumia mwaliko wa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa tamthilia yako ya Mbaya Wetu tarehe tatu Juni mwaka wa elfu kumi na nne (3/6/2014). Hafla yenyewe ilifanyika kwenye ukumbi wa Alliance Française jijini Nairobi. Hatukuonana tu! Tulisalimiana kwa mikono. Mashabiki wako walikuwa wengi ishara kuwa Prof, ulipendwa.

Maigizo ya tamthilia hiyo yalivutia kiasi kwamba nilikosa kutoka ukumbini kabla ya uigizaji kutamatika ili nirudi nyumbani. Matokeo? Nilikosa magari ya kurudi Ongata Rongai. Ilifika saa sita usiku nikiwa kwenye stendi, ndipo nikajua nilikuwa nikiwatekenya sinzia. Nilisema na bawabu fulani akakubali tulinde lango naye hadi kulipoanuka. Pengine nilistahili kujuta na kujutia ila sivyo ilivyokuwa. Ningejuta vipi ilhali nilikuwa nimekutana nawe? Isitoshe, ulikuwa umenipa nakala ya Mbaya Wetu uliyoitia sahihi mwenyewe.

1f

Prof, tarehe 26/4/2017 tulikutana tena kwenye ukumbi ule ule wa Alliance Française. Ilikuwa hafla ya kumtangaza mshindi wa Tuzo ya Ubunifu, 2016. (Tuzo iliyoshindwa na Ngulamu Mwaviro; ilidhaminiwa na Nation Media Group, Spotlight Publishers na Ubalozi wa Ufaransa nchini Kenya). Ilikuwa fahari na furaha kuwa miongoni mwa waandishi walioshindania tuzo hiyo. Ingawa sikuimbuka mshindi, nilifurahia sana kuuona mswada wangu wa Wimbi la Mabadiliko ukiwa kati ya kumi na tano bora. Mbegu uliyoatika ndani yangu ilikuwa imeanza kuota. Ujumbe wako siku hiyo, kwa niaba ya jopo, ulitutabiria siku njema kwetu sote.

Mara ya mwisho kukutana nawe ilikuwa Jumamosi, Oktoba 14. 2017 ndani ya ukumbi wa Huduma ya Maktaba kwa Taifa eneo la Buruburu. Hapa tulipata nafasi nzuri ya kuyasema mengi. Hakika uliniambia mengi baada ya kuniuliza, “Je, unaendelea kuandika?”
Nilikuahidi kukupokeza nakala ya riwaya yangu mara tu ingechapishwa—umeondoka kabla ya hilo kutimia.

Ukumbini ulisema, “Wewe ni mwandishi. Endelea kuandika. Hata wachapishaji wakisita kuchapisha si hoja; watakuwa tu wamefeli kutekeleza wajibu wao. Usijishughulishe na yasiyokuhusu. Lako ni kuandika tu.”
Prof, makala yako ya Kina cha Fikra, Kauli ya Walibora haikunipita hasa Alhamisi na baadaye Jumatano, hadi leo. Nakumbuka ukiyanukuu maoni yangu kwenye gazeti la Taifa Leo kuhusu tatizo letu la ‘kutoionea fahari lugha yetu ashirafu ya Kiswahili’. Hilo lilikuwa kubwa! Mwaka mmoja baadaye, ukawa unayasoma mashairi yangu kwenye gazeti lilo hilo la Taifa Leo. Nilipokosea ulinikosoa.

Siku ya mwisho kuwasiliana nawe ulinitajia mswada wako ambao ulitamani kuuona ukiwa umechapishwa. Mswada wa Barack Obama: Ndiyo, Twaweza. Sina habari kabla ya kuondoka kwako shughuli ya uchapishaji ilikuwa imefika wapi. Ulinihimiza kuwa na subra. Eti nisikate tamaa kwani hata nawe husubiri. Miswada yako pia huchukua miaka kabla ya kuchapishwa, sembuse yangu? (Sisi chipukizi). Uliongeza kuwa umewahi kufeli na kuteleza, sawa na binadamu wengine ulimwenguni. Muhimu ni kutokata tamaa… yalikuwa yako ya mwisho kwangu.

Prof, ulalapo salama, Waswahili tutakukumbuka. Mchango wako katika tasnia mbalimbali hutofutika. Tutaikumbuka kauli yako ya ‘kutopigania fito…’ Tutayapeza makala yako gazetini. Siku moja, siku moja Prof, Kenya itapata Baraza la Kiswahili ili makala yako ya mwisho kuandika ipate pumzi.

Sina mengi. Hatuna mengi. Lala pema, tutaonana baadaye.

Dennis Shonko, 15/4/2020

2 thoughts on “@DennisShonko LALA PEMA PROF. KEN WALIBORA: INGAWA UMEONDOKA, HUTAFUTIKA MOYONI MWANGU.

  1. Nilikisoma kitabu chake ken walibora ambacho ni kidagaa kimemuoz katika shule ya upili mtakatifu Elizabeth-sibakala na nilifunza mambo mengi Sana kulingana na wahusika kama Amani,Imani, mwalimu majisifu,Mtemi Nasaba Bora na wengine…..mungu ailaze roho yake Mali pema……

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s