@DennisShonko NILIVYODHALILISHWA KWA KUZUNGUMZA LUGHA YA KISWAHILI

interview

Mwalimu na wanafunzi ofisini.

Nakumbuka namna mvua ilikuwa inatunyeshea mchana kutwa tulipokuwa safarini (usiulize tulikuwa na nani. Hayo ni ya siku nyingine). Safari ya kutoka jijini Nairobi kuelekea eneo la *Kiduni. Usishangae kuwa kunyesha kwa mvua hiyo hakukuitia imani yangu baridi. Baridi iliyokusudia kutugeuza kuku aliyenyonyolewa chini ya pepo zitokazo pande zote duniani. Ninachojaribu kusema ni kwamba, nilikuwa katika safari ya kwenda kuonja kipande kingine cha maisha au bora niseme, kuandika ibara nyingine ya maisha yangu.

Baada ya saa kadhaa za kusumbuana na utingo, tulifika katika Chuo cha Ualimu cha *Nira. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuingia humo, sikwambii kufika Kiduni. Watu wachache walikuwa bado wamepiga foleni wakisubiri ima kusajiliwa rasmi chuoni au kuwashika mikono wana wao katika shughuli hiyo nzima. Nilijua sikuwa na kila kitu kilichokuwa kinahitajika; si vitabu si si idadi tosha ya pesa. Ile kauli ya ‘mtu hujikuna ajipatapo’, nilijua haingenifaa wakati kama huo. Nilikuwa kama mbuzi mbele ya hakimu chui! Hebu nisonge mbele kidogo…

Nililazimika kuingia kwenye ofisi ya mwalimu mkuu ili nijieleze na kutoa sababu zangu za kutolipa koto wala karo iliyohitajika. Nilifaa kufanya uamuzi wa busara tena wa harakaharaka. Nirudi nyumbani na kusubiri mwaka mwingine mmoja au niingie humo ofisini nipatane na nisiyemjua sura, jina wala jinsia. Nani asubiri mwaka mwingine mmoja?

Hali ofisini.

Come in!” Ndiyo kauli iliyonifikia pale mlangoni nilipokuwa nimesimama. Hapo ndipo niliusikia mpigo wa moyo wangu ambao nilikuwa nimekazana kuupuuza kwa muda. Ilikuwa ni kama ngoma za msondo hasa! Nikaingia. Macho yangu yalikutana na uso wa bibi mmoja aliyekuwa amekula akashiba (ikiwa kusema hivyo ni sahihi). Pandikizi la mtu! Nilishindwa nianzie wapi nimalizie wapi. Ninachokumbuka ni namna nilivyomuamkua, ‘shikamoo’. Nilikuwa na mazoea ya kuamkuaamkua watu niliowajua na nisiowajua. Nayo mazoea yana taabu ati. Na hiyo kauli niliithibisha siku hiyo nilipojibiwa kwa kuulizwa swali; “You don’t know how to speak in English? Which village are you from?” Sikuyaamini masikio yangu. Niliumwa! Nikameza mate machungu kama shubiri.

I-I know ma-ma-madam,” nilijitetea kwa kudodosa maneno.

Then speak!” na kweli nilisema. Nilisema sana! Ila katika huko kusema sana nina uhakika sikuomba msamaha kwa kutamka neno la Kiswahili. Nikidhani Kiswahili ni lugha ya taifa tena rasmi. Je, ndivyo inavyosema katiba yetu? Niandikapo makala hii, nina katiba ya nchi yetu mezani. Naipitia sura ya pili, ibara ya saba ya katiba– sijui mara ya mia ngapi. Na natumai unajua nimekuwa nikijaribu kusoma nini.

Baadaye basi, aliniambia nimwandikie barua kuhusu ombi langu. Ombi la kutaka kuongezwa muda wa kulipa karo. Na ingekuwa hatia iwapo ningeandika katika Kiswahili. Keshoye asubuhi na mapema, nilikuwa mlangoni pake. Alinipata hapo na barua mkononi. Akanikaribisha ndani. Nikamkabidhi barua, akaisoma. Kisha kwa tabasamu akatamka, Wow! I can see you are very good in English.” Ajabu! Sasa bibimtu alikuwa na maneno ya halua. Aliniuliza maswali mengi ambayo yalichangiwa na kushangaa kwake huko kuhusu umilisi wangu wa lugha ya Kiingereza. Mwisho wa yote, nilitoka ofisini mwake nikiwa na tabasamu na mwingi wa maswali. Maswali kuhusu ‘kosa’ langu la kuzungumza Kiswahili. Lugha hii itumiwe na kina nani? Itumiwe wapi? Mtu akisema kwa Kiswahili aripuriwe viboko visivyohesabika au achomwe kwa maji moto? Mustakabali wa matumizi ya Kiswahili sanifu ni upi jamani?

Hebu nimeze funda la mate…

6 thoughts on “@DennisShonko NILIVYODHALILISHWA KWA KUZUNGUMZA LUGHA YA KISWAHILI

  1. Sitaki kubanika matukio ya siku yenyewe hapa. Hilo halina natija katu. Lakini nataka kusisitiza kuwa msururu wa Tamasha hizo umekuwa na ufanisi mkubwa si tu katika maandalizi bali pia katika kufaulisha dhima kuu yake-kukuza lugha ya KISWAHILI.
    Mjo na uwepo wa wajuzi wa lugha kutoka sehemu tofauti, wenye vitembo tofauti na mitazamo tofauti kuhusi l;u

  2. Lugha na mawanda yake. Mimi kwa maoni yangu nahisi kuwa ikiwa makongamano kama haya yatatiliwa mkazo , basi yatafanikisha kwa akali Fulani makuzi ya lugha na mustaakabali wa Kiswahili.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s